Pages

Baada ya Kuongoza Mgomo na Kutesa Watanzania: BP yauzwa kwa Puma

KAMPUNI ya Mafuta ya BP Tanzania Limited, imewaomba radhi Watanzania na Serikali kutokana na kufanya mgomo wa kutoa huduma ya mafuta ikipinga fomula mpya iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).  BP iligoma kuuza bidhaa yake kwa kutumia fomula hiyo takriban mwezi mmoja uliopita kwa madai kuwa ingekuwa inauza chini ya gharama halisi na hivyo kupata hasara kubwa.  Kutokana na hatua hiyo, Ewura iliifungia leseni na hivyo isijihusishe na biashara hiyo kwa miezi mitatu.

Uamuzi ambao haukukubaliwa na BP hivyo ikaamua kukata rufaa Mahakama ya Ushindani Kibiashara (FTC).  Mkurugenzi Mkuu wa BP Tanzania, Engelhardt Kongoro, amesema kuwa wakati EWURA inachukua uamuzi wa kuifungia kampuni hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ilikuwa inashauriana na wanahisa wa kampuni hiyo, kuomba ruhusa ya kama wauze mafuta hayo kwa bei ya hasara au la.  “Tulifanya hivyo, kwa vile Bodi haina mamlaka ya kuuza bidhaa zake kwa bei ya chini hadi inapopata ruhusa kutoka kwa wanahisa,” alisema Kongoro.

Wanahisa wa kampuni hiyo ni Serikali ya Tanzania na Kampuni ya BP ya Uingereza. Kongoro alisema baada ya kuchelewa kupata ruhusa kutoka kwa wanahisa, hawakutekeleza agizo la Ewura, hali ambayo ilifanya ifungiwe kuuza bidhaa zake Agosti 12. Kampuni ya BP kwa sasa imeuzwa kwa Puma Energy Tanzania Investiment Limited, ambayo imeonesha kusikitishwa na hatua zilizochukuliwa na wawekezaji hao wa zamani, ambazo ni wazi kuwa zilikiuka sheria na taratibu za nchi.

“Kwa hali hiyo, BP Tanzania inapenda kuwaomba radhi Serikali ya Tanzania, Ewura, Watanzania na wateja wetu kwa jumla, kwa usumbufu uliojitokeza wakati tuliposimamisha huduma zetu,” alisema Kongoro.

Mkurugenzi huyo alisema kutokana na uamuzi huo wa kuomba radhi, BP Tanzania imewaagiza wanasheria wake kufuta kesi zote mbili ilizofungua FCT.  Kongoro alisema wakirejeshewa leseni yao, wawekezaji wapya; Puma Energy, itaendelea na biashara ya mafuta kama kawaida na itauza bidhaa hiyo kwa bei ya Serikali.  Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema Bodi ya Ewura itairejeshea leseni kampuni hiyo itakapotimiza masharti.

Moja ni kuwaambia wananchi kwa nini waligoma kuuza mafuta, kuomba radhi kwa wananchi, kufuta kesi na kulipa gharama za kesi hiyo. Wakati huo huo, BP Tanzania imetangaza rasmi kuuzwa kwa kampuni hiyo kwa Puma Energy kuanzia mwezi huu. Kwa hatua hiyo, Puma itamiliki asilimia 50 ya hisa na Serikali kiasi hicho hicho. Novemba Puma na BP Afrika zilikamilisha taratibu za kuuzwa kwa hisa za BP katika nchi tano zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania.

Kwa hali hiyo, baada ya taratibu kukamilika, Puma ndiyo itakuwa inaongoza menejimenti ya BP wakati taratibu za makabidhiano zikiendelea kufanywa katika ngazi mbalimbali.



http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21228&cat=kitaifa