Pages

CHADEMA MATATANI: Hijab ya DC sasa moto

WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikisema hakiwezi kutoa tamko la kulaani tukio la kuvuliwa hijab Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario kulikofanywa na wafuasi na viongozi wake, Waislamu nchini wamekuja juu.

Mbali na hao, mbunge mmoja amekitaka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kuvunja ukimya kuhusu kudhalilishwa kwa mwanamke huyo aliyekuwa akitekeleza majukumu yake.

Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) kupitia Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba, imelaani udhalilishaji huo.

Baraza, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shura ya Mashehe mkoani Tabora, pia imelaani udhalilishaji dhidi ya DC Kimario na kutamka kuwa kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na Waislamu wote nchini.

Katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, Mufti alisema Bakwata halikusudii kuingilia uhuru wa kampeni za vyama vinavyohusika katika uchaguzi wa Igunga, bali kutetea haki ya msingi ya mwanamke wa Kiislamu ambaye kwa mujibu wa ubinadamu,

Katiba ya nchi na imani ya dini yake, amedhalilishwa na kudhulumiwa haki yake ya msingi na uhuru wa imani yake.

“Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania linalaani kwa nguvu zake zote kitendo alichofanyiwa mama Kimario kwani si tu kwamba kimemdhalilisha na kumfedhehesha mama huyo, pia kitendo hicho kinaashiria dharau ya hali ya juu kwa utamaduni wa Kiislamu,” alisema Mufti na kuongeza:

“Bakwata inapenda kuwaasa viongozi wa kisiasa kwamba masuala ya kidini yasiwe ndio yanayowaongoza katika kutafuta ridhaa ya kuingia madarakani. Watafute ridhaa hiyo kwa kunadi sera za vyama vyao katika njia ya kistaarabu na kiungwana.

“Waislamu tuko macho kuhakikisha kuwa udini unaoendeshwa na Chadema unakemewa ipasavyo ili kulinda hali ya utulivu na amani Tanzania.”

Kwa upande wake, katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jana Igunga, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Ally Kondela, alisema kitendo kilichofanywa na chama hicho ni kuudhalilisha Uislamu.

Taarifa iliendelea kueleza kuwa chama cha maendeleo chadema kimedhihirisha wazi kuwa
kina chuki na dharau dhidi ya waislamu tangu mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu.

“Waislamu tunatamka wazi hatuna imani na chama hicho, viongozi tunaomba Waislamu wote
wasikipigie kura Chadema na tunawaomba wananchi wote wapenda amani wasikipigie kura,” ilisema taarifa ya Sheikh Kondela.

Ilisema taarifa hiyo kwamba Waislamu wa Tabora wameshitushwa, kufadhaishwa na kusikitishwa na tukio lililotokea katika kampeni za Uchaguzi Mdogo Jimbo la Igunga kwa kuvuliwa hijab mama wa Kiislamu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Zarina Madabida (CCM), ameitaka Tawla kuvunja ukimya ulionao juu ya tukio la kudhalilishwa DC Kimario.

Akizungumza juzi, Madabida alisema alichofanyiwa Kimario ni kitendo cha aibu na kinyama ambacho Tawla pamoja na asasi zingine zinazoshughulikia masula ya wanawake hazikupaswa kukaa kimya.

“Tunafahamu kuwa tayari vyombo vya kisheria vinavyohusika vimelichukulia hatua suala hili, lakini ninapata shida kuona watetezi wa haki za mwanamke wakinyamaza kimya pasi na kukemea suala, jambo linalotufanya tushindwe kufahamu kawa sababu gani,” alihoji
Madabida.

Kwa upande wake, Chadema imesema hakiwezi kutoa tamko la kulaani tukio linalomhusu DC Kimario kwa vile suala hilo liko mahakamani.

Mshauri wa Mambo ya Sheria wa chama hicho, Profesa Abdallah Safari alisema ushahidi utakaotolewa mahakamani ndio utakaothibitisha kama mkuu huyo wa wilaya alivaa hijab ama hakuvaa na kama alivaa, alivuliwa kwa bahati mbaya ama kwa makusudi.

“Sio vizuri viongozi wa dini kutoa hukumu kwa suala ambalo liko kortini. Korani inasema Inallah Maswabirina (Mungu yuko pamoja na wenye subira)... Masheikh wanaijua aya hii kwa nini katika suala hili hawakufanya subira? Somo hili kwao limeenda wapi…kuna nini hapa?

Akiwa na mwanasheria mwingine wa Chadema, Mabere Marando, alisema wanaamini kuwa tamko la wanazuoni juu yao ni njama za wazi zinazofanywa na CCM kuwafarakanisha Waislamu na Chadema katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mdogo Igunga.

“Hii ni kampeni ya wazi kwa CCM na sisi tunasema chama chetu kina wafuasi wa dini zote. Tunao Wakiristo, Wapagani na Waislamu wazuri wenye staha ambao wanaipigia debe Chadema. Kwa kweli tumesikitishwa na kauli hii ya masheikh,” alisema.

Alisema chama chake kinamlalamkia DC Kimario kwa vile alikuwa anapanga hujuma za kuihujumu Chadema wakati wa uchaguzi.

Viongozi watatu wa Chadema wakiwamo wabunge wawili wamefikishwa mahakamani Tabora, wakikabiliwa na mashitaka manne ya wizi wa simu, shambulio, matusi ya nguoni na utekaji nyara. Kesi yao imeahirishwa hadi Oktoba 10.