Pages

Mgawo wa umeme kupandisha bei ya bia

KAMPUNI ya Bia nchini (TBL) imesema iwapo mgawo wa umeme utaendelea nchini, italazimika kupandisha bei za bidhaa zake. Licha ya kutosema kiwango cha upandaji huo, kampuni hiyo imesema italazimika kupandisha bei kutokana na sasa kuna ongezeko kubwa la ankara ya umeme na mafuta na kuwa mara tano zaidi ya ile ya awali kwa mwaka.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa TBL, Phocus Lasway alisema wanaishauri Serikali kuchukua hatua thabiti ili kuhakikisha kuna mipango ya muda mfupi na mrefu wa kuhakikisha tatizo la umeme linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.“Tatizo la umeme linarudisha nyuma ukuaji wa uchumi nchini, gharama za uzalishaji zinakuwa juu, ajira zinapotea, na hivyo kufanya usalama wa wananchi kuwa hatarini”, alisema.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL, Gavin van Wijk, alisema kuwa kampuni hiyo imeingia gharama kubwa kwa kununua majenereta na pia kuongeza gharama za umeme na mafuta kila mwaka kutokana na kutokuwepo uhakika wa umeme.  “Kutokana na tatizo la umeme nchini, kampuni yetu imelazimika kuongeza mtaji wetu mara mbili ili kuweza kuzibeba gharama za uendeshaji bila ya kumuathiri mtumiaji,” Gavin alisema.

TBL imetumia kiasi cha dola za Kimarekani milioni 2.4 kwa ajili ya kununua jenereta kubwa la kuzalishia umeme kwa ajili ya kiwanda cha mkoani Mwanza.

Mbali na hilo, Gavin alisema kuwa TBL ilitumia kiasi cha dola milioni moja kwa ajili ya manunuzi ya jenereta ya kiwanda cha Arusha. Naye Meneja wa kiwanda cha TBL, Dar es Salaam, Salvatory Rweyemamu, alisema kuwa gharama za uendeshaji zimezidi kuongezeka siku hadi siku kutokana na tatizo la umeme nchini.

Kila saa moja wanapotumia jenereta wanatumia kiasi cha lita za mafuta ya dizeli zipatazo 400.

Meneja wa Kiwanda cha TBL, Mbeya, Calvin Martin, alisema “mgawo wa umeme unaathiri kwa kiasi kikubwa kampuni ingawa imeamua kwa sasa kubeba gharama zote za ziada kwa kupunguza matumizi yake badala ya kumbebesha mlaji gharama hizo kwa kuongeza bei za
bidhaa zake. Ila tunatumia jenereta kwa uzalishaji wa bidhaa zetu.”

Kutokana na tatizo hilo, Lasway ameishauri Serikali kuachana na uzalishaji umeme kwa kutumia majenereta ya kukodishwa na kuwekeza kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali asilia.