Pages

Waislamu waing’ang’ania Chadema

Katibu wa Sekretarieti ya Wanazuoni, Sherally Huseein (kulia) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)kukataa kuomba radhi kwa Waislamu kufuatia udhalilishaji wa kumvua hijabu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora, Fatma Kimario hivi karibuni.


ZIKIWA zimebaki siku tano ufanyike uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Igunga mkoani Tabora, Umoja wa Wanawazuoni wa Kiislamu (HAY-AT), umewataka waumini wa dini hiyo kutoiunga mkono Chadema na kuiona kama ukoma.

Akitoa tamko hilo jana Dar es Salaam, Katibu wa Umoja huo - Maulamaa, Shehe Hserally Hussein alisema Chadema ina sera isiyo rasmi ya kuhujumu Uislamu nchini.

Hatua hiyo inatokana na Chadema kukiuka agizo la Umoja huo, uliowapa siku tatu kulaani kitendo cha wafuasi na viongozi wake, kulidhalilisha vazi tukufu la hijabu na kumwomba radhi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, kwa kumvua sitara yake.

“Tunatoa agizo kwa mujibu wa kanuni inayomtaka Mwislamu, kupambana na wale wote wenye kupiga vita Uislamu na kuacha kuwasaidia kwa namna yoyote ile, hadi pale watakapoomba radhi na kuacha kuidhalilisha dini hiyo,” Shehe Hussein aliwaambia waandishi wa habari jana.

Alisema Umoja huo haukuwa na nia ya kuchukua msimamo huo dhidi ya Chadema, bali umelazimishwa na msimamo hasi wa chama hicho kuhusu hijabu ambayo ni moja ya mafundisho ya Kiislamu.

Alisema Chadema imeonesha wazi dharau kwa vazi la hijabu, kwa kukataa kuomba radhi na kusema si jambo la kutolewa tamko na kujipa mamlaka ya kutafsiri mafundisho ya Uislamu kuhusu hijabu, jambo ambalo hawana elimu nalo.

Alisema licha ya kuongeza siku ili chama hicho kiombe radhi, wao walijibu kwa kejeli kupitia kwa wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wao, Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando na Tundu Lissu, wakisisitiza kuwa hawataomba radhi, huku wakidai uchunguzi wao, inaonesha kuwa Kimario hakuvaa hijabu.

Aidha, walitoa shutuma za uongo kwa mashehe waliosimama kutetea hijabu na heshima ya mwanamke wa kiislamu, kuwa wanatumia nyadhifa zao kupotosha waumini na hawajui maana ya vazi hilo.

“Tunapenda kuwaweka wazi, kuwa Profesa Safari ni msomi wa sheria za kisekula na si msomi wa dini ya kiislamu, hivyo hana haki ya kuwa mfasiri wa mambo ya dini, wenye hadhi na maarifa ya kutafsiri kilichovaliwa kama ni hijabu au la ni wanazuoni, kwa kuwa tuna elimu ya dini,” alisema Shehe Hussein.

Alisema wanatoa tahadhari kwa mwenendo wa Chadema kujichukulia sheria mkononi, kuwa wamejipa mamlaka ya vyombo vya Dola kuchunguza, kukamata na kutoa adhabu kwa wanaowaona kuwa ni wahalifu kama walivyofanya kwa Mkuu wa Wilaya.

“Suala tunaloshughulikia si kama mama huyo ana hatia au la au Chadema wametenda kosa hilo au la, bali ni kitendo walichomfanyia yule mama, wamelidhalilisha vazi tukufu la hijabu ambalo ni alama miongoni mwa alama za kidini,” alifafanua Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Mohammed Issa.

Kwa mujibu wa Issa, Chadema wanaona hijabu ni vazi linalofunika mwili mzima na kuacha macho, jambo ambalo si kweli kwani hijabu ni stara katika mwili hata kofia ni hijabu kwa mwanamume.

“Mtandio ni hijabu, hata watawa wa kikristo vitambaa wanavyovaa ni hijabu, lakini kwa lile vazi linaloacha wazi uso linaitwa jaris au juribabu na nchini Afghanistani watu huvaa vazi kama hilo liitwalo burqa,” alisema Issa alipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita.

Septemba 15, viongozi wa Chadema na wafuasi wao walimvamia na kumkamata Kimario wakati akifanya mikutano ya ndani na viongozi wa matawi, vijiji na kata, wakidai alikiuka taratibu na kwamba alikuwa na lengo la kuhujumu chama hicho.