Pages

Mjane wa Habyarimana kutorejeshwa Rwanda

Agathe Habyarimana
Mahakama ya Ufaransa imekataa ombi la Rwanda la kumsafirisha mjane wa aliyekuwa rais Juvenal Habyarimana, ambapo kifo chake kilichochea mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Rwanda inamshutumu Agathe Habyarimana, mwenye umri wa miaka 69, kwa kusaidia kupanga mauaji ya kimbari. Amekana mashtaka hayo. 

Waziri wa sheria wa Rwanda Tharcisse Karugarama ameiambia BBC kuwa anaheshimu uamuzi huo, lakini amesema sasa anakabiliwa na kesi Ufaransa. Zaidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa kati 800,000 waliuawa kwenye mauaji hayo. 

Juvenal Habyarimana, Mhutu, aliuawa baada ya ndege yake kudunguliwa karibu na uwanja wa ndege wa Kigali Aprili 6, 1994. Katika kipindi cha saa chache vurugu, zilizoanzishwa zaidi na Wahutu dhidi ya Watutsi, zilienea kuanzia mji mkuu mpaka nchini kote. 
Juvenal Habyarimana
Wanamgambo wa Kihutu waliwalaumu Watutsi kwa kudungua ndege hiyo ya Rais, licha ya kwamba mpaka leo haijathibitishwa nani alihusika. Inaaminiwa kwa kiasi kikubwa kuwa Wahutu wenye msimamo mkali na serikali walishapanga mauaji hayo muda mrefu sana.