Pages

Moto wateketeza mitambo ya Star media Dar es Salaam

MITAMBO na jenereta vya Kampuni ya Starmedia, Bamaga, Dar es Salaam vimeteketea kwa moto baada ya kutokea hitilafu katika transfoma iliyowekwa na Tanesco saa mbili kabla.

Kampuni hiyo inayohusika na uuzaji wa ving’amuzi, iko katika Jengo la Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mkurugenzi wa Starmedia, William Lan, alisema moto huo ulioanza saa nane kasoro, chanzo chake kinahisiwa kuwa ni hitilafu za kiufundi zilizosababishwa na transfoma hiyo iliyofungwa jirani na chumba kilichoteketea, saa mbili kabla ya kuzuka kwa moto huo.

Alisema hana hakika ni lina matangazo ya kupitia kwenye king’amuzi, yataanza kurushwa tena hadi hapo watakapofanya ukaguzi wa mitambo iliyopo ili kubaini imeathiriwa kiasi gani na moto huo.

Aidha, alisema ni mapema mno kueleza hasara iliyopatikana wala chanzo cha moto huo, japo anahisi kuwa umesababishwa na transfoma hiyo, ambayo alisema atawasiliana na Tanesco ili waiondoe katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Usambazaji Umeme wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alisema kwa namna tatizo lilivyo, wanahisi kusababishwa na hitilafu ya kiufundi baada ya kufungwa kwa transfoma hiyo.

Alisema wataunda Tume itakayowahusisha watu kutoka Starmedia, Polisi, TBC, Kikosi cha Zimamoto ili kuchunguza chanzo cha tatizo hilo, japo hakueleza muda itakayotumia kukamilisha shughuli hiyo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela aliyekuwepo katika eneo la tukio, alisifu jitihada zilizochukuliwa na vikosi vya uokoaji vikiongozwa na Kikosi cha Jiji, Ultimate, Polisi kwa namna vilivyofanikisha kudhibiti madhara zaidi ya moto huo.