Pages

Mauaji makubwa yafanyika Burundi

Takriban watu 36 wameuawa baada ya watu wenye silaha wasiojulikana kufyatua risasi kwenye baa iliyojaa watu karibu na mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, maafisa wamesema.
Wamesema idadi ya waliofariki dunia inaweza kuongezeka kwani watu wengi wamejeruhiwa vibaya kwenye uvamizi huo eneo la Gatumba.

Kundi la mwisho la waasi la Burundi lilisalimisha silaha zao rasmi mwaka 2009 lakini mashambulio ya hapa na pale yamekuwa yakiendelea. Mwandishi wa BBC Prime Ndikumagenge mjini Bujumbura amesema ni shambulio baya kabisa kutokea tangu uchaguzi kufanyika mwaka jana. Aliyekuwa mkuu wa waasi Agathon Rwasa alijitoa kugombea urais na kukimbia baada ya chama chake cha National Liberation Forces (FNL) kuishutumu serikali kwa udanganyifu.
Serikali imelaumu mashambulio ya hivi karibuni kufanywa na magenge lakini mwandishi wetu alisema baadhi wanahofia huenda kundi jipya la waasi limeibuka.

Miili kwenye maegesho ya magari

" Idadi kubwa ya watu, baadhi wakiwa wamevaa sare za kijeshi na bunduki aina ya Kalashnikov na maguruneti yaliingia kwenye baa ya 'Chez les Amis'.Mmoja aliyenusurika lakini akapoteza ndugu zake wawili na rafiki mmoja aliliambia shirika la habari la AFP, "Walimwambia kila mmoja alale chini na kuanza kupiga risasi."

Daktari aliyetoa jina lake moja la Leonard alisema hospitali anapofanyia kazi "ilizidiwa" na idadi ya majeruhi.
AFP inaripoti kwamba miili ya watu iliachwa kwenye maegesho ya magari katika hospitali moja.
Rais Pierre Nkurunziza alitembelea eneo lilipofanyika shambulio hilo huko Gatumba na kuahidi kuwachukulia hatua kwa wale waliohusika.Alisema ameahirisha safari yake ya wiki hii ya mjini New York, ambapo kutakuwepo mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Takriban watu 300,000 wanadhaniwa kuuawa nchini Burundi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 12 baina ya Watutsi walio wachache lakini ndio waliokhodhi jeshi na waasi wa Kihutu.Mapigano hayo yaliisha rasmi mwaka 2005 kwa makubaliano ya amani yaliyomshuhudia kiongozi wa waasi Pierre Nkurunziza kuchaguliwa kuwa Rais lakini waasi wa FNL wameendelea kupigana.


http://www.bbc.co.uk/swahili/habari/2011/09/110919_burundi.shtml