Pages

Wabunge Chadema wapanda kizimbani

WABUNGE wawili na Mjumbe wa Baraza la Vijana la Chadema, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Tabora, wakikabiliwa na mashitaka manne likiwamo shambulio na kumshikilia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, kinyume cha sheria.

Waliofikishwa mahakamani hapo jana ni Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga na Mjumbe wa Bavicha Wilaya ya Igunga, Anwar Kashaga. Watatu hao walifikishwa mahakamani hapo saa 4.55 asubuhi kwa gari la Polisi na kuingizwa katika chumba cha mahabusu saa 5.05, huku umati wa wananchi ukiwa umefurika katika Mahakama hiyo.

Ilipofika saa 5.16, washitakiwa hao walipandishwa kizimbani huku wakipunga vidole viwili kuonesha ishara ya ‘V’ inayotumiwa na Chadema.

Walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa, Thomas Simba na waendesha Mashitaka wa Serikali, Juma Masanja na Mugisha Mbonea.

Masanja alidai kuwa Septemba 15 mchana katika kijiji cha Isakamaliwa, Igunga, Kasulumbai alidaiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Kimario.

Alidai pia kwamba mshitakiwa huyo alimtukana Mkuu huyo wa Wilaya kwa kumwita kuwa ni
“malaya mkubwa … ndiye niliyetaka kuzaa naye, mpumbavu mkubwa na Mkuu gani wa Wilaya asiye na akili.

Hayo yalikuwa ni mashitaka ya kwanza kwa Mbunge huyo ambayo alisomewa peke yake na kukana.

Mwendesha Mashitaka aliendelea kudai kwamba siku hiyo, katika kijiji cha Isakamaliwa, washitakiwa wote walimshambulia Kimario na kumsababishia maumivu kichwani.

Katika mashitaka ya tatu, kwa pamoja walimshikilia Mkuu huyo wa Wilaya isivyo halali.

Kwenye mashitaka ya nne yanayohusu watuhumiwa wote watatu ambao wanatuhumiwa kufanya wizi wa maungoni, wakidaiwa kumwibia Kimario simu ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya Sh 400,000.

Wote walikana mashitaka. Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu akisaidiwa na Wakili wa Kujitegemea, Musa Kwikima, waliomba Mahakama iwape dhamana washitakiwa, kwa kuwa kosa hilo si kubwa na hawana shaka yoyote
kwani hawezi kutoroka ikizingatiwa kwamba washitakiwa wawili ni wabunge wa Bunge la Tanzania.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliiomba Mahakama kwamba ikiwezekana wabunge hao wajidhamini kwani hawawezi kutoroka kwa nafasi walizonazo katika Bunge; lakini upande wa mashitaka ulikataa ombi la kujidhamini.

Hakimu Simba naye alitupilia ombi hilo na kutaka washitakiwa kila mmoja adhaminiwe na wadhamini wawili kwa Sh milioni tano kwa maneno, ambapo wote walitimiza masharti ya dhamana na wako nje kwa dhamana hadi Oktoba 10, kesi hiyo itakapotajwa.

Hata hivyo, Mahakama iliwaonya washitakiwa hao wasitende kosa lolote la jinai litakalosababisha kufikishwa mahakamani kipindi chote kesi itapokuwa mahakamani, vinginevyo, itafuta dhamana yao.

Wabunge hao walikamatwa na Polisi mjini Igunga, Septemba 16 na kuhojiwa kisha wakaachiwa huru, kabla ya kukamatwa tena siku iliyofuata na juzi kuletwa hapa kujibu tuhuma zao.

Baada ya kuachiwa kwa dhamana, watuhumiwa wote walipanda gari la Lissu na kwenda moja kwa moja Igunga kuendelea na kampeni.

Kimario anadaiwa kuvamiwa na wafuasi wa Chadema pamoja na wabunge hao wawili
alipokuwa akifanya mkutano wa kikazi katika eneo hilo la Isakamaliwa, ambapo alivuliwa hijab na mtandio wake, kuibiwa simu na kudhalilishwa.

Katika hatua nyingine, washitakiwa hao watatu jana walipokewa na wafuasi wao mjini Igunga takriban 500 wengi wao wakiwa ni vijana.

Hata hivyo, katika mapokezi hayo, kijana mmoja aliomba kujaribu kuimba wimbo na alipopewa kipaza sauti, akaimba, ''Kama sio nguvu zako Kikwete, Rostam angetoka wapi?'', wimbo ambao ulimsababishia zahama kwani alipigwa na ikabidi akafichwe kwenye gari la matangazo, baada ya kutaka kupigwa zaidi akidaiwa ni mwanaCCM.
 
http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21085