Pages

Meli tano zapigwa marufuku Zanzibar

MAMLAKA ya vyombo vya baharini Zanzibar, zimesimamisha huduma za meli tano kutokana na meli hizo kutokidhi viwango vinavyotakiwa kusafirisha abiria na mizigo.

Meli zilizositishwa safari ni Mv Serengeti, Nura, Buraq One, Buraq Two pamoja na Mubarak kutokana na usajili wa meli hizo ulikuwa ni kusaidia kuvuta meli baharini (tagi) na siyo kubeba abiria.

Akitoa taarifa hizo kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Mamlaka wa Vyombo vya Bahari Zanzibar, Haji Vuai Ussi alisema kukatishwa kwa safari kwa vyombo hivyo kumetokana na kukosa usalama wa uhakika kwa abiria wake.

Aidha, alisema ingawa meli hizo zilianza kazi za kuchukua abiria kwa muda mrefu, lakini zilishindwa kujisajili kwa kazi hiyo, jambo ambalo limekuwa likienda kinyume cha taratibu za vyombo vya bahari.

Vuai alisema meli hizo pia zilikuwa zikihudumiwa na wafanyakazi wasiokuwa na sifa wala taaluma ya ubaharia pamoja na kushindwa kutoa taarifa za usalama kwa wasafiri wakati wanapokuwa safarini.

Alisema Mamlaka imebaini tatizo kubwa katika meli hizo baada ya kufanya ukaguzi na kugundua kuwa meli zote hizo zimekosa mfumo mzuri wa mawasiliano pale linapotokea tatizo la kiufundi.

Akizungumzia kuhusu usalama wa vyombo vya baharini kwa ujumla, alisema mamlaka imegundua pia matatizo lukuki kwa manahodha wa meli hizo kwa kuondoa meli bila kujua taarifa za usalama wa abiria wao.

Mkurugenzi huyo alisema mamlaka yake imejipanga upya kuhakikisha kuwa wanachukua hatua za kisheria kwa nahodha ye yote ambaye atabainika kuondoa meli bila ya kuwa na taarifa sahihi za abiria.

Hivyo amewataka wamiliki wa vyombo vya baharini kutoa ushirikiano kwa mamlaka.