Pages

Prof. Tibaijuka ataka fidia wanaobomolewa ipande

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewaagiza maofisa ardhi kuandaa viwango vipya vya ulipaji fidia wananchi ambao ardhi yao inachukuliwa na Serikali, ili viendane na bei ya soko.

Amesema wananchi wamekuwa wanalalamikia fidia wanayolipwa kuwa ndogo, hali ambayo imechangia migogoro mingi kutokana na wananchi kugomea fidia husika, hivyo kuchelewesha
uendelezaji wa baadhi ya maeneo.

Alisema hayo jijini Dar es Salaamwakati akifungua mkutano wa sekta ya ardhi unaohusisha watathmini wa ardhi, maofisa ardhi, wapima ardhi, maofisa mipango miji na wasajili wa hati.

Wengine ni wenyeviti wa mabaraza ya ardhi na nyumba na wasajili wa mabaraza hayo, kutoka wizarani, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji.

Aliwataka maofisa hao baada ya mkutano huo, kupeleka mapendekezo wizarani yanayohusu mbinu mpya za kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, bila kuathiri waliopo hususani wanaomiliki ardhi.

“Mjadili namna gani wananchi hawatakuwa masikini zaidi kutokana na utekelezaji wa mipango yenu na mbinu bora za kutathmini na kulipa fidia na kuangalia viwango vya fidia.

“Tutende haki katika kulipa fidia, tuandae viwango na tuviwasilishe serikalini haraka na nawaahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi haraka, maana watu wanataka kufaidika na ardhi yao hawataki migogoro,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alitoa agizo hilo kutokana na fidia wanayolipwa wananchi kuhusu mazao, nyumba na ardhi inayochukuliwa na Serikali, kuzua malalamiko mengi.

“Viongozi tupo hapa kupambana na umasikini na si kupambana na masikini,” alisema Waziri.

Aliwataka watendaji hao kujipanga kuhakikisha wanaifanya ardhi kuwa moja ya njia kuu za uchumi na mtaji wa kweli kwa mwananchi wa kawaida.

Katika hotuba yake, Waziri pia aliwataka watendaji wa sekta hiyo, kujitathmini na kujiandaa kubadili mwonekano wao miongoni mwa jamii, kutokana na kujulikana kama mafisadi wa ardhi.

Alisema watumishi wasio waadilifu wajiondoe kabla hawajaondolewa.

Alisema hali imefikia hapo kutokana na baadhi ya watendaji wanaoongozwa na malengo binafsi, badala ya kuongozwa na sheria, kanuni na taratibu za utendaji, hali ambayo imesababisha utoaji huduma kwa wateja kuwa chini ya kiwango na ukusanyaji hafifu wa maduhuli ya Serikali.

Waziri pia alisema katika kipindi cha miezi 11 aliyokaa wizarani pamoja na Naibu wake wamegundua kuwa baadhi ya matatizo hayo hayasababishwi na watendaji wa sekta hiyo; bali ni mashinikizo kutoka kwa vigogo walioko serikalini.

Aliwataka watumishi hao kuwa wajasiri wakatae kutekeleza maagizo ambayo yanavunja sheria.

“Simamia maadili ya kazi yao, kama akija Mkuu wa Mkoa, Waziri au Baraza la Madiwani kukushinikiza ufanye jambo kinyume na maadili, mwambie wazi kuwa hilo halitekelezeki.”

Aliwataka waache tabia ya kukubali kila jambo wanaloelekezwa na wakubwa wao badala yake waende kuripoti wizarani kuhusu suala hilo.

“Mimi si mbabaishaji, hata aliyeniweka hapa anajua hilo, hivyo nawaambieni msiwe watu wa ‘ndiyo mzee’ katika utendaji wenu, nyie si yatima mna wizara inayohusika na masuala hayo.”

Kuhusu migogoro ya ardhi, Profesa Tibaijuka alisema wizara yake inaandaa fomu za ugawaji wa ardhi ambazo zitakuwa na kipengele ambacho mbunge na diwani wa eneo husika, lazima asaini kabla ya mwekezaji kukabidhiwa ardhi ya eneo husika.

Alisema kitendo cha viongozi hao kushiriki kugawa ardhi, kutasaidia kupunguza migogoro na malalamiko kwa viongozi hao na wananchi wenyewe.

Kuhusu maeneo ya wazi, alisema kuanzia sasa wataweka matangazo katika maeneo hayo ili ambao wamejenga watambue kuwa muda wowote watabomolewa na hati zao zitabatilishwa.

Aliishangaa halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kuwa imekuwa ikisubiri wizara ichukue hatua za kwenda kubomolea watu wakati jukumu hilo ni lao.

“Hawa ambao wamejenga maeneo ya wazi malalamiko yao mwisho ni kwangu, hata kwa rais
hayafiki hivyo msiwabembeleze.”

Aliikemea tena Manispaa ya Kinondoni kuwa hali ya ufisadi inatisha, hadi Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Mipango Miji walitaka kufungwa, kutokana na madudu yanayofanywa na manispaa hiyo.

“Nyie Kinondoni mambo yenu si mazuri, nitakuja kula chakula pamoja nanyi tuzungumze,” alisema Waziri.