Pages

SAKATA LA MAHITA KUZAA NJE: Mahita akubali yaishe, amlipa mwanae mil.9/

ALIYEKUWA Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omar Mahita amekubali kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kuhusu mtoto aliyekuwa akimkataa kwamba si wake.

Jana Mahita alilipa Sh milioni tisa kupitia kwa wakili wake, Charles Semgalawe na kuahidi kulipa Sh milioni tatu zilizobaki baada ya siku 30 kuanzia jana.

Mahita alikubali kulipa gharama za matunzo ya mtoto huyo, Juma Mahita tangu mwaka 2003 hadi hukumu ilipotolewa Septemba mwaka juzi.

Fedha hizo amezilipa kupitia Kampuni ya Udalali ya Nasm Auction Mart iliyoamriwa na Mahakama ya Wilaya Kinondoni kuuza mali za Mahita ili fedha hizo zipatikane.

Uamuzi wa mahakama ulitokana na Mahita kugoma na hivyo mama wa mtoto, Rehema Shabani kurudi mahakamani na kutoa taarifa.

Mtoto huyo Juma Mahita kwa sasa anasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Hananasif Kinondoni.

Kabla ya kulipa fedha hizo, Kampuni hiyo ya udalali, ilimpa Mahita notisi ya siku 14 iliyomalizika jana.

Awali Mahakama ya Kinondoni ilitoa hukumu ambayo ilimpa ushindi mlalamikaji (mama wa mtoto) na kutamka kuwa Juma ni mtoto halali wa Mahita.

Mahakama ilimtaka Mahita alipe gharama za matunzo ya mtoto huyo tangu mwaka 2003 hadi siku ya hukumu.

Mahakama hiyo pia ilimtaka Mahita kulipa Sh 100,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto huyo baada ya kulipa Sh milioni 12 hizo.

Hata hivyo, Mahita alikata rufaa kupinga hukumu hiyo. Rufaa ilitupiliwa mbali na mahakama kumuamuru amri ya mahakama iliyotolewa awali ya kumtaka kulipa fedha hizo, itekelezwe.

Katika uamuzi wa rufaa hiyo, Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu, alisema Mahakama ya Kinondoni ilikuwa sahihi. Alimtaka Mahita kulipa pia gharama za kesi hiyo.