Pages

UHABA WA SUKARI TANZANIA: JWTZ kurithi Polisi katika kuzuia usafirishaji wa sukari nje

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewatuhumu polisi, kwamba wanahusika na utoroshaji wa sukari nje ya nchi na kulitaka Jeshi hilo kukomesha vitendo hivyo mara moja, vinginevyo Serikali italiagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuingilia kati ili kudhibiti vitendo hivyo.

Akiwahutubia mamia ya wakazi wa hapa akiwa katika ziara ya Mkoa wa Mara, Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kulikalia kimya suala hilo huku wananchi wakiteseka.

Alisema viwanda vya sukari vya Mtibwa na Kilombero vilivyopo mkoani Morogoro, Kagera na TPC cha Moshi, vinafanya kazi nzuri ya kuzalisha wastani mzuri wa sukari ambayo
inatosha kwa matumizi ya wananchi, lakini sukari hiyo haipatikani nchini.

“Viwanda hivi vinazalisha tani 41,000 hadi 44,000 wakati matumizi yetu ni wastani wa tani 30,000 na 31,000; hii inaonesha kwamba kuna karibu tani zaidi ya 10,000 za ziada. Lakini jambo la ajabu sukari haipatikani nchini na kuifanya kupanda bei na kuumiza wananchi,” alisema Pinda.

Alisema amepewa taarifa za siri, kwamba baadhi ya polisi wanashiriki katika utoroshaji huo wa sukari kwenda nchi jirani na husindikiza magari ya wafanyabiashara yenye sukari ili kupita kwenye vizuizi vya barabarani kirahisi.

“Wanapigiana hadi simu kutaarifiana, kwamba jamani eee kuna gari lenye namba fulani linakuja na mzigo, likifika hapo lipite bila matatizo.

Wanafanya hivi kwa maslahi yao binafsi na si kuwasaidia Watanzania. “Nimemwagiza RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) na kundi lake, lakini pia nimemwagiza Kaimu Mkuu wa Mkoa (Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Geofrey Ngatuni) kukomesha suala hili haraka.

Kama itaonekana wanashindwa, basi tutawaagiza Jeshi (JWTZ) kuingia kati ili kudhibiti. “Hatutaki kufika huko, nawaomba polisi wafanye kazi yao ipasavyo ili kukomesha hali hiyo mara moja,” alisema Pinda.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali itaendelea kuipa ushirikiano mkubwa sekta binafsi ili kuiwezesha kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Alisema wakati Serikali ikichukua hatua hiyo ya kushawishi uwekezaji, itajitahidi pia kuhakikisha kuwa wawekezaji wanaojitokeza ili kuwekeza nchini hawawaonei wananchi.

“Lazima tuwatie moyo ili wazidi kuwekeza nchini. Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha tunafanya kila jitihada wasituonee. Wapo wawekezaji ambao wao wanaangalia faida tu wanataka watuonee na kutudhibiti, hawa hatutawakubali,” alisema Pinda.