Pages

Airtel kuwafidia wateja wa Blackberry

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imetangaza kuongeza siku tatu za ziada kwa wateja wake wote wanaotumia huduma ya Blackberry kutokana na tatizo la mtandao lililotokea hivi karibuni na kuathiri mtandao wa intaneti kwa Blackberry duniani kote.

Tatizo lililoathiri mtandao tayari limesharekebishwa na watoa huduma hiyo kwenye mtandao wa blackberry na imegundulika kuwa tatizo hilo lilisababishwa na hitilafu iliyoathiri mfumo wa mtandao wa kutuma ujumbe na peruzi kwa njia ya mtandao duniani kote lililodumu kwa siku tatu mfululizo.

Tatizo hili lilianzia Ulaya na kuzikumba pia nchi za Mashariki ya Kati, Afrika na India kisha kusambaa Kaskazini mwa Amerika.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Sam Elangallor ilisema, “Tunasikitishwa sana na tatizo lililowakumba wateja wetu wanaotumia huduma ya blackberry hivi karibuni, hivyo leo naomba niwajulishe wateja wetu wote yaani wa malipo kabla na baada tunawaongezea siku tatu kuendelea kutumia huduma hiyo bila malipo mara baada ya kifurushi cha mwezi Oktoba kuisha.”

Mkurugenzi huyo aliongeza, “Tutaendelea pia kuwajulisha wateja wetu wote kuhusu kuongezewa siku hizi tatu kupitia njia ya sms ili kila mmoja afahamu kuwa fidia imefanyika kwa tatizo alilopata.”

Alisema wateja wa malipo baada, ambao hulipa ankara zao kila mwisho wa mwezi, pia wataongezewa siku tatu katika huduma ya blackberry kwa mwezi huu. Ongezeko la kutumia huduma ya blackberry bila malipo kwa siku tatu kwao litaonekana katika taarifa zao za malipo zinazotolewa kwao kwa Oktoba, alisema.

Alisema Airtel inatambua kuwa tatizo la kukosekana kwa mtandao kwa wateja wake wanaotumia huduma za blackberry halikusababishwa na mitambo ya Airtel, bali hitilafu iliyotokea kwenye mtandao duniani kote, hivyo kuona umuhimu wa kuwarudishia wateja wake huduma bure kwa siku hizo walizokosa.

  



 
http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=22138