Pages

Utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja waiva

UTARATIBU uliokuwa unasubiriwa kwa muda mrefu wa uagizaji wa mafuta kwa wingi kwa
pamoja, sasa uko katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.

Chini ya utaratibu huu, kampuni ya mafuta itakayoshinda zabuni ya uagizaji mafuta nchini, itatakiwa kuingiza bidhaa za petroli zitakazokidhi mahitaji ya taifa kwa kipindi fulani na sio kama ilivyo sasa ambapo kila kampuni inaingiza bidhaa hizo kama inavyotaka.

Pia kampuni za mafuta zitaruhusiwa kushirikiana ili kukidhi mahitaji chini ya mpango huu mpya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni iliyo na jukumu la kuratibu mpango huu mpya, Petroleum Importation Co-ordinator Ltd (PIC LTD), Salum Bisarara alisema kwa sasa zinatafutwa kampuni zitakazokua na uwezo wa kuleta wastani wa tani za ujazo 150,000 kwa mwezi chini ya utaratibu huu mpya.

“Mpango mzima unaendelea vizuri,” alisema Bisarara na kuongeza kwamba meli ya kwanza kuingiza mafuta chini ya utaratibu huu mpya inatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu ya Desemba mwaka huu.

Akifafanua zaidi, alisema utaratibu wa kutafuta kampuni hizo unafuata taratibu za kimataifa na sheria za nchi.

Miezi michache iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA), Haruna Masebu, alisema utaratibu wa kununua mafuta kwa pamoja na kwa wingi ungeanza kutumika muda wowote nchini kuanzia mwezi wa tisa mwaka huu.

Mamlaka hiyo ilisema kwanza taratibu zote zilizotakiwa kuwepo zilikua zimeshakamilika.

Kama moja ya matayarisho hayo, tayari Ewura ilishawasiliana na kituo cha kupakulia mafuta cha Kurasini (KOJ) ili kipanue sehemu ya hifadhi ya mafuta kuendana na mahitaji ya utaratibu huo mpya.



http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=22057