Pages

MABOMU TENA: Mkulima afukua mabomu shambani

MWANAMKE mkulima wa Kijiji cha Kalembwa wilayani Bukombe mkoani Shinyanga, juzi alinusurika kufa baada ya kulima shamba lililokuwa limezikwa mabomu ya kivita yanayotumiwa vitani kwa kurushwa kwa mkono.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi jana, tukio hilo limetokea juzi saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Kalembwa wakati mwanamke huyo, Christina Sizya (80) alipokuwa akilima shambani kwake.

Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga, Diwani Athumani alisema ofisini kwake jana kuwa Chiristina akiwa analima shambani kwake, aliona vitu asivyovifahamu baada ya kuwa amelima shamba hilo karibu nusu ekari tangu alfajiri alipoanza kulima shamba hilo.

“Chiristina alitoa taarifa za vitu hivyo asivyovifahamu Polisi na muda mfupi baadaye polisi walifika eneo la tukio kabla mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono yaliyogundulika shambani humo hayajaleta madhara kwa binadamu,’’ alisema Kamanda Athumani.

Alisema mabomu hayo yalikuwa yamefukiwa ardhini shambani na mtu au watu wasiofahamika kwa lengo la kutaka kuyatumia katika matukio ya vitendo vya uhalifu kinyume cha sheria.

Kamanda huyo wa Polisi alimpongeza mwanamke huyo kwa kuwa makini na moyo wa ujasiri kwa kutoa taarifa Polisi kwa wakati unaotakiwa, kabla madhara makubwa hayajatokea kwa wananchi wa eneo hilo.

Alitoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa za siri zitakazowezesha kukamatwa kwa mtu au watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ili wakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu makosa yanayowakabili kwa mujibu wa sheria za nchi.