Pages

Mwakyembe apelekwa India

Mh. Rais akimjulia hali Dr. Mwakyembe

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe amepelekwa katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu baada ya hali ya afya yake kuwa tete kwa kuugua ugonjwa unaomsababishia kuvimba mwili wake.
 
 Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), alikiri kuwa Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, anasumbuliwa na maradhi hayo na amesafirishwa jana kwenda India kwa matibabu zaidi.

“Ni kweli Mheshimiwa Waziri ameondoka leo (jana) mchana na ndege ya Qatar Airline kwenda India kwa matibabu zaidi,” alisema Mwambalaswa ambaye kama Dk. Mwakyembe anatoka mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Mwambalaswa, hali ya Dk. Mwakyembe si mbaya sana kwa kuwa anaweza kula na kutembea vizuri ingawa bado amevimba baadhi ya sehemu mwilini.

Dk. Mwakyembe anadaiwa kusumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis na alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo zaidi ya miezi mitatu iliyopita, lakini kwa sasa hali ya ugonjwa huo imezidi kuwa mbaya.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda alisema hana taarifa za kuugua kwa Dk. Mwakyembe kwa kuwa alikuwa safarini, lakini aliahidi kuzungumzia suala hilo baada ya kupata ripoti zaidi.

Mwakyembe alizungumza juzi na gazeti moja la kila siku na kukiri kuwa anaumwa na kwamba hata sura yake imebadilika huku akikanusha madai ya kulishwa sumu.

Ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe unadaiwa huathiri wanaume na wanawake wenye umri kuanzia miaka 55 na dalili zake ni kuwashwa, mwili kuishiwa nguvu na sehemu ya juu ya ngozi kupukutika.

Chanzo cha ugonjwa huo hakijajulikana, lakini kinahusishwa na magonjwa ya ngozi na madhara ya matumizi ya dawa mbalimbali. Hospitali ya Apollo aliyopelekwa Dk. Mwakyembe, ndiko alikolazwa Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya kwa muda mrefu sasa, baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo, ambaye kwa sasa hali yake imeelezwa kuendelea vizuri.

Juzi, Rais Jakaya Kikwete alikwenda kumjulia hali Dk. Mwakyembe nyumbani kwake Kunduchi jijini Dar es Salaam.






source: http://www.habarileo.co.tz/