Kwa muda mrefu sana suala la barabara za jiji la Dar es salaam limekua kikwazo kikubwa cha usafiri na usafirishaji. Yani hili suala mimi binafsi huwa linanikereketa sana sana. Standard ya barabara zetu ni mbovu sana, na karibia barabara kuu zote zipo katika hali mbaya, ya mashimo makubwa barabarani ambayo mara nyingine yanasababisha ajali na pia uharibifu mkubwa wa magari.
Baadhi tu ya maeneo sugu ambayo mimi hupita kila siku ni pamoja na barabara inayopita Mwananyamala hospital. Yani hii barabara ina mahandaki! manake mashimo hayo ni makubwa kupita kiasi. Mimi najiuliza hivi mwananyamala hamna diwani? Hakuna mbunge? Hakuna hata katibu kata jamani? ina maana wahusika wa barabara ile hawaoni? watendaji je? Juzi, Bonge wa 88.4 clouds FM aliamua kupanda migomba kwenye barabara hii, kuonyesha tu ukubwa wa mashimo haya. Hivi ni kweli kwamba watendaji wetu lazima tuwasukume kufanya kila kitu? Na wananchi wa mwananyamala ilhali wakijua hilo mbona bado wanendelea kuwapa madaraka?
Mtangazaji wa clouds fm maarufu kwa jina la Bonge akipanda mgomba kwenye barabara ya mwananyamala karibu kabisa na geti linaloingia hospitali ya mwananyamala. (Picha kwa hisani ya Michuzi blog) |
Eneo lingine ni makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela (pale taa za ubungo) yaani kati kati ya taa zile kuna bonge la shimo, limechimbika kiasi kwamba ukikosea kidogo tu ukaliingia vibaya unaweza kuacha tairi, na hii ni kati ya barabara muhimu sana manake ndio barabara kuu ya kutoka nje ya mji kuelekea mikoani. Sasa swali langu mimi ni kwamba hivi hakuna waheshimiwa wanaotumia barabara hii? na Tanroads wao wanasemaje kuhusiana na suala hili?
Eneo lingine ni hii bara bara ya Mpya ya bagamoyo, kuanzia makutano ya Bamaga hadi Morocco kupita mbele ya Millenium towers, hii barabara nayo ina mashimo yaliyochimbika sana ambayo na yenyewe yanasababisha watumiaji wa magari kuingia hasara za utengenezaji wa magari yao kila baada ya muda mfupi. Mvua ikinyesha sasa inakua balaa zaidi. Siku moja mimi mwenyewe nimewahi kukaa kwenye foleni kutoka kinondoni morocco pale hadi Bamaga nilitumia masaa matano. Kweli tena sitanii, nilikua Morocco saa kumi na mbili na nusu na nilifika Bamaga saa nne usiku. Hii ilikua siku ya mvua, tena si zaidi ya mwezi na nusu uliopita. Swali langu sasa, Tanroads wanafanya kazi gani? na wenye jengo lao lile la Millenium towers "LAPF" mfuko huu wa pensheni wa serikali umeshindwa kabisa kufanya kazi yake kwa jamii inayowazunguka? where is the Corporate social responsibility hapo?
Haya sasa, tuje old bagamoyo road. Kuanzia Morocco hadi round about ya kawe pale, Mheshimiwa Halima Mdee upo????. Hii nayo haifai. tena maeneo ya kuanzia shoppers kupita DTP na TMJ hospital hadi BP petrol station pale ndio worse, yani barabara ina mahandaki manake sio mashimo haya. Tena barabara hii mvua ikinyesha unaweza ukavua samaki kabisa, maji yanajaa haifai, halafu kuna ki-daraja mchwara pale baada tu ya Shoppers ambacho mvua ikinyesha tu basi huwa kanafurika na magari ya watu yanadumbukia chini ya daraja. Watu wengi sana wameumia pale kwenye haka kadaraja, mimi mwenyewe nimewahi kushuhudia bajaji ikidumbukia na kuzama kabisaa, ni bahati tu kwamba dereva na abiria wake hawakupata serious injuries.
Tuje kwenye barabara ya Masaki kupitia St. Peters hadi mwisho kule seacliff. Hii barabara sijui chini kuna mkondo wa maji au chemichemi? manake kila siku kuna ibuka mashimo mapya, wanajitahidi wanazibaziba lakini yanaibuka mapya kila siku. Hadi barabara hii inayoingia uzunguni siku hizi ina mashimo sasa kwingine tutapona kweli?
Unajua ni lazima viongozi wetu wote wa ngazi za kisiasa na za kiutendaji wakumbuke kua usafirshaji ni moja ya sekta amabzo ni uti wa mgono wa taifa lolote, haswa katika mataifa yetu yanaondelea. Mfanyakazi au mwananchi anapotumia masaa mawili kwa safari ambayo ingetumia nusu saa au chini ya hapo anakua ameipotezea nchi mapato na kasi ya maendeleo ambayo ingepatikana kama muda huo ungetumika kwenye masuala ya maendeleo. Wageni wengi wanokuja nchini kwetu wote hukwazwa sana na foleni na pia hukwazwa zaidi na suala la kwamba watanzania huwa hatuna haraka. Na huu utamaduni wa kutokua na haraka umejengeka kuanzia mabarabarani mwetu. Mtu ambae anakaa Mbezi tu hapo, ili afike kazini kwake saa moja Lazima atoke nyumbani kwake saa kumi na nusu. Sasa fikiria angefika kazini saa kumi na mbili, maendeleo ya aina gani tungekua nayo leo.
Mimi najisemea tu jamani, likikuchoma lifanyie kazi.