Jamani hii sio haki kabisa, kodi zilivyopanda hivi halafu kuna watu wanalipia kodi nyumba za Umma halafu hawazikalii? Halafu eti wanabishana kabisaa hawataki wenyewe wakague nyumba zao
Source : http://www.mwananchi.co.tz/biashara/-/15464-baadhi-ya-nyumba-nhc-hazikaliwi-watafiti
SIKU chache baada ya Watanzania wenye asili ya kiasia kuja juu na kuonyesha hofu yao juu ya utafiti unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linalohoji masuala mbalimbali ikiwamo asili yao, watafiti wanaoendesha utafiti huo kwa niaba ya shirika hilo, wamebaini kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu za upangaji licha ya hatua kadhaa zilizochukuliwa kudhibiti tatizo hilo.
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza katika utekelezaji wa kazi hiyo iliyoanza Agosti 15 mwaka huu, ni baadhi ya wapangaji kuhodhi nyumba bila kuzitumia inangawa wanazilipia pango kwa kila mwezi.
Mmoja wa watafiti hao ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Felician Komu, aliwaambia wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jan kuwa baadhi ya nyumba zilikuwa hazina kituo na kwamba hiyo inaonyesha kuwa wamezihodhi bila kuzitumia.
Hali hiyo inajitokeza wakati NHC ikiwa tayari imefuta mikataba 379 ya upangaji baada ya uhakiki uliobaini kwamba baadhi ya wateja wake, walikuwa wamepangisha nyumba hizo, kinyume cha sheria.
Badala yake NHC iliamua kuingia mikataba ya upangishaji na wale waliokutwa ndani ya nyumba hizo, kwa kuwatoza asilimia 90 ya kodi waliyokuwa wakitozwa kinyemela kila mwezi.
Dk Komu alisema pamoja na kasoro hiyo, utafiti huo wanaoufanyika katika nyumba zote za NHC kote nchini, unaendelea vizuri na kwamba wapangaji wengi wanajitokeza kujibu dodoso.
"Tumepata mwitiko mzuri, hadi sasa hakujawa na matatizo makubwa, wapangaji ambao hakuwakuta wakati tulipokuwa tunapita katika nyumba walizopang, walijitokeza na kuja katika ofisi zetu kujaza dodoso kwa hiyari yao,"alisema Dk Komu.
Alisema tayari walishapitisha dodoso kwa zaidi ya wapangaji 1,600 katika maeneo ya Temeke, Ilala na Magomeni jijini Dar es Salaam, maeneo ambako utafiti huo umeanzia.
Kwa upande wae, Dk Tatu Limbumba wa chuo hicho, alisema utafiti huo unafanywa na timu ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Adhi waliomaliza mwaka wa nne, wakisimamiwa kwa karibu na wahadhiri saba ambao ni wataalamu wa masuala ya usimamizi wa majumba na wengine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema katika utafiti unaoilenga jamii kama ilivyofanywa na NHC, kuna masuala ya msingi yanayozingatiwa na yanayozaa dodoso ambazo hazikuwa na lengo la kumbagua mtu au vinginevyo.
Mkurugenzi wa Miliki wa NHC, Hamad Abdallah, alisema utafiti huo unalenga katika kupata taarifa muhimu za kila mpangaji na kuliwezesha shirika kuwa na takwimu sahihi.Alisema utafiti huo hauna lengo la kumbagua Mtanzania yeyote kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
"Utafiti ni wa kisayansi na tumewapa wataalamu waweze kutufanyia kazi hiyo, tunataka tupate taarifa muhimu za wapangaji ili tutakapofikia hatua ya ujenzi wa nyumba 15,000 tujue tunamjengea mteja wa aina gani, kwani kila mteja ana matakwa yake, mathalani mteja mzungu ana ladha zake, mwafrika vile vile pia akiwa wa asili ya kiasia anayo matakwa yake,"alisema.
Alisema pia kwamba lengo la shirika hilo ni kuwapa Watanzania wengi zaidi, fursa ya kumiliki nyumba na kupata upangaji katika nyumba hizo za umma
Source : http://www.mwananchi.co.tz/biashara/-/15464-baadhi-ya-nyumba-nhc-hazikaliwi-watafiti