Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, Mkuu wa utumishi wa Umma Francis Muthaura na aliyekuwa mkuu wa polisi Jenerali Hussein Ali watafika mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai iliyoko the Hague Uholanzi ICC.
Viongozi hao wanatuhumiwa kupanga ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya. Zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine 500,000 walilazimika kuhama makaazi yao. Mahakama hiyo inaanza kupokea ushaidi kuthibitisha ikiwa watu hao watafunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kivita. Viongozi wanaofika mahakamani leo ni washirika wa karibu wa Rais Mwai Kibaki. Ghasia zilizuka baada ya wafuasi wa Rais Mwai Kibaki kutuhumiwa kujaribu kuvuruga uchaguzi wa urais. Ghasia hizo zilimalizika wakati Bw Kibaki na hasimu wake Raila Odinga kukubaliana kugawana madaraka, huku Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu.
Kulingana na mwandishi wa BBC mjini the Hague Peter Musembi, mwendesha mashtaka Louis Moreno Ocampo atawasilisha ushaidi wa watu kumi ambao wanasema Bw Kenyatta na Bw Muthaura walipanga mikutano na kundi haramu la Mungiki ilikuandaa mashambulizi ya kulipisha kisasi. Naibu Waziri Mkuu, ameamua kutoa ushaidi wake mwenyewe na atahojiwa na mawakili wa pande zote.
Kwa upande wake mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura na aliyekuwa kamishna wa polisi wanapinga kesi hiyo dhidi yao kwa misingi kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuwafungulia mashataka.
Waziri wa zamani wa Elimu ya juu Wiliam Ruto, waziri wa zamani wa Viwanda Henry Kosgey na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang ni washukiwa wengine ambao walihusishwa na chama cha waziri mkuu Raila Odinga.
Washukiwa hao walifika mahakamani mapema mwezi huu kujibu mashtaka ya kupanga ghasia hizo na kusababisha maafa hayo.