Get Paid To Promote, Get Paid To Popup, Get Paid Display Banner

Watuhumiwa mv Spice Islander waachiwa kwa dhamana

WATUHUMIWA watatu kati ya wanne waliofikishwa kwenye Mahakama Kuu mjini Zanzibar wiki iliyopita wakikabiliwa na kosa la uzembe na kusababisha vifo vya watu 203 waliokuwa wakisafiri kwa meli ya mv Spice Islander usiku wa kuamkia Septemba 10, na kuzama katika Bahari ya Hindi, wamepewa dhamana.

Watuhumiwa waliopewa dhamana ni Abdallah Mohammed Ali (30) mkazi wa Bububu, ambaye ni Ofisa Mkuu wa meli ya mv Spice Islander na Yussuf Suleiman Jussa (47), mkazi wa Kikwajuni ambaye pia ni mmoja wa wamiliki wa meli na Msimamizi Mkuu wa Mizigo katika meli hiyo.

Mwingine ni Simai Nyange Simai (27) mkazi wa Mkele ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Mamlaka ya Usafiri Baharini akihusika na usalama wa abiria melini.

Watuhumiwa hao, Ijumaa iliyopita walirejeshwa rumande baada ya kuzuka mabishano ya kisheria ya kutaka wapewe dhamama au la, ambapo Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Kazi, aliamuru warejeshwe rumande hadi jana atakapotoa uamuzi.

Walipofikishwa mahakamani hapo, Wakili wa Utetezi, Hamidi Ali Mbwezeleni aliiomba Mahakama iwaachie huru watuhumiwa hao ili Tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza chanzo
cha kuzama kwa meli hiyo iendelee na kazi yake la sivyo, Tume isitishe kazi yake hadi pale kesi itakapomalizika.

Wakili huyo alisema kutakuwa na utata kama watuhumiwa wataendelea kubaki rumande kwani watakosa haki yao ya msingi katika Tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar wakati ikiendelea na kazi yake endapo itataka kupata taarifa ama maoni kutoka kwa watuhumiwa hao hivyo wakiwa
mahabusu watakosa haki yao ya kujieleza mbele ya Tume hiyo.

Alisema hivi sasa inaonekana kuna makundi mawili yanayofanya kazi moja kwa maana ya Mahakama na Tume jambo ambalo alisema litakuwa na utata na lenye makusudio ya kuwalinda baadhi ya watu fulani.

Hata hivyo, ingawa Mwanasheria wa Serikali Ramadhani Ali Nassib alitetea uamuzi wa kutaka watuhumiwa hao wabaki rumande wakati Tume ikiendelea na kazi yake, Kazi alikubaliana na hoja ya utetezi na kuamuru watuhumiwa hao wawe nje kwa dhamana hadi Tume ya Rais itakapomaliza kazi yake.

Watuhumiwa wote watatu walipewa dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 na wadhamini wawili kila mmoja kwa kiasi hicho hicho.

Watuhumiwa waliondoka huku mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Saidi Abdallah Kinyanyite (58) ambaye alikuwa nahodha wa meli ya mv Spice Islander akiendelea kusakwa na Polisi.

source: http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21088