Get Paid To Promote, Get Paid To Popup, Get Paid Display Banner

Kikwete atunukiwa tuzo mbili UN

RAIS Jakaya Kikwete amepokea tuzo mbili maalumu kwa mchango wake mkubwa katika afya ya mjamzito na mtoto, kutoka taasisi mbili tofauti jijini hapa.

Tuzo ya kwanza imetolewa na Taasisi ya Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UN Foundation) na kukabidhiwa kwa Rais na Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo anayeshughulikia sera ya Umma,
Peter Yeo.

Ya pili ilitolewa katika makao makuu ya Soko la Hisa la Marekani (NASDAQ) ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani baada ya lile la New York. Rais alikabidhiwa tuzo hiyo jana na Makamu
wa Rais wa NASDAQ, David Wicks.

Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Rais alipewa heshima maalumu ya kugonga kengele kuashiria mwisho wa biashara siku hiyo.

Akipokea tuzo hizo mbili, Rais Kikwete alielezea changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini na Afrika kwa jumla na kuzishukuru nchi na taasisi ambazo zinaunga mkono juhudi za kupunguza matatizo ya afya ya mjamzito.

“Si sahihi kwa mjamzito kufariki dunia wakati anampa uhai binadamu mwingine, uzazi unatakiwa kuwa shughuli ya furaha na si huzuni na ndiyo maana tumetoa kipaumbele kwa afya ya mjamzito kwenye ajenda yetu ya afya,” Rais alisema.

Aliwaeleza wageni waalikwa ambao katika hadhara zote mbili walitoka nchi na taasisi mbalimbali, kuwa kati ya vitu ambavyo Serikali ya Awamu ya Nne imeamua kutoa kipaumbele ni kuongeza huduma za afya ya uzazi kwa kujenga zahanati na kuzipandisha daraja zilizopo.

Serikali pia inaajiri wakunga na wataalamu zaidi wa afya na kuongeza mafunzo katika sekta hiyo. Juhudi zingine ni pamoja na kutoa huduma za Mpango wa Uzazi bure na kutoa vifaa vya kujifungulia kwa akinamama wanaohudhuria kliniki.

“Vifaa hivi ni maalumu kwa ajili ya kusaidia akina mama wakati wa kujifungua, na tunaamini kuwa kwa kufanya hivyo, wanawake wengi zaidi watahudhuria kliniki na kuwapa motisha wa kujifungulia katika taasisi zetu za afya,” alisema Rais.

Kutokana na juhudi hizo, takwimu zinaonesha kupungua kwa vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua, kutoka 8,000 mwaka 2005 hadi 6,000 mwaka jana.

“Upungufu wa vifo 2,000 ni hatua nzuri katika muda mfupi, lakini bado hairidhishi sana, tunaweza kupunguza zaidi na hilo ndilo lengo letu, kwani hatutaki kuona mwanamke anakufa kutokana na ujauzito au kujifungua,” alisema.

Mbali na shughuli hizo, Rais pia alizungumza na Rais wa Slovenia Dk. Danilo Turk, Makamu Waziri Mkuu wa Luxembourg, Jean Asselborn na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na Waziri wa Maendeleo wa Uingereza, Andrew Mitchell.

Jana Rais Kikwete alitarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.


http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21229