Get Paid To Promote, Get Paid To Popup, Get Paid Display Banner

JAMANI WAMASAI MLIOSOMA KOMBOENI WENZENU BASI

WANAFUNZI wa kike 12 kutoka jamii ya wafugaji ya Kimasai waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kupangiwa kusoma Shule ya Sekondari ya Parakuyo wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, wameozeshwa kwa siri.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ndoa hizo zilifanyika kimila na lengo ni wazazi wao kujiongezea mifugo.

Wakati wanafunzi hao wakiozeshwa, wazazi wasiopenda kupeleka watoto wao wa kike shuleni, wamesherehekea uhamisho wa aliyekuwa Mkuu
wa Mkoa huo, Issa Machibya, aliyekuwa akiwafuatilia.

Kutokana na kushamiri kwa tatizo hilo, wanaharakati wa jamii hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wamelazimika kuwafichua wazazi wanaowaozesha watoto wao wa kike na waoaji akiwemo mfugaji wa kabila hilo, aliyetajwa kwa jina la Lepolosi Sinyagwa mwenye umri kati ya miaka 50 na 55.

Mfugaji huyo anatuhumiwa kumwoa kuwa mke wa nne, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa), aliyefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kutakiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza kwenye sekondari hiyo maalumu kwa wafugaji.

Baada ya wanaharakati hao wa jamii ya Kimasai wa vijiji vya Parakuyo na Twatwatwa, kufikisha taarifa ya mfugaji huyo kwa Uongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Kilosa, hatua ya kumkamata zilichukuliwa, lakini alitoroka kabla ya kukamatwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kijijini hapo hivi karibuni, walidai kuwa watoto wengi wa kike wanaozeshwa ili
kupata mifugo ‘ng’ombe’ kwa lengo la kuongeza himaya ya mifugo.

Gazeti hili lilifika hadi katika makazi ya mtuhumiwa, ambapo lilikuta maboma matatu ya mfugaji huyo bila mwenyewe kuwapo huku akiwa amewatelekeza wake zake na watoto baada ya kuwakimbia polisi ambao walikuwa wakimsaka.

Mmoja wa wake zake aliyekuwepo nyumbani hapo, alipoulizwa aliko mumewe, alikataa kuzungumza akitumia mkalimani.

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Parakuyo, Agnes Mataya, alisema watoto wa kike ndiyo wanaopata shida wanapohitimu darasa la saba pamoja na kufaulu, wazazi wamekuwa wakiwatorosha kuwapeleka maeneo ya mbali ili baadaye waozeshwe tofauti na wa kiume ambao wao
wanafanyishwa kazi ya kuchunga.

“Hili ni tatizo kubwa katika vijiji vya wafugaji wa jamii yetu, mtoto wa kike anapochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari,
njama zinafanyika na baadhi ya wazazi ya huwatorosha kwenda sehemu za mbali ili baadaye waweze kuozeshwa kwa wanaume wa jamii hiyo kwa tamaa ya kupata ng’ombe wengi,” alisema.

“Watoto wanafaulu sana katika shule zetu za msingi, lakini bado wengi hasa wasichana wanachepuka pembeni, wanatoroshwa na
wazazi wao ili waozeshwe na jambo hilo halifuatiliwi kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji kuhusika nalo.”

Naye Mzee Kafuna Steti wa jamii hiyo, alisema wazazi wanaopindisha njia kwa kuwaozesha watoto wa kike waliochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari wakiwemo na wavulana kuwapatia kazi ya kuchunga mifugo, Serikali iwachukulie hatua za kisheria.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Parakuyo alisema wanafunzi wengi waliochaguliwa kujiunga shuleni hapo hawaripoti wote.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Parakuyo, Lekileng’o Kibasisi, akiri kuwepo kwa wanafunzi wa kike waliofaulu kujiunga na sekondari mwaka jana, kutoroshwa kwenda kuolewa kinyume cha sheria; lakini alikanusha uongozi wake kufumbia macho suala hilo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego, akizungumzia jambo hilo, alisema mkakati uliopo sasa ni kufanya msako utakaowezesha kuwapata wanafunzi hao 12 ili warudishwe kuendelea na masomo.

Katika hatua nyingine, wafugaji wa jamii ya Kimasai katika kijiji hicho cha Parakuyo, wamesherehekea kuhamishwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Issa Machibya.

Hatua hiyo imetokana na Machibya aliyehamishiwa Kigoma, kuvalia njuga suala la wazazi wa jamii hiyo wanaowaozesha watoto wao wa
kike waliofaulu mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.

“Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa Machibya kufika kijijini hapa na kutoa maelekezo ya kukomesha suala la kuwaozesha wanafunzi wa kike, wenye kuendeleza tabia ya kuozesha wanafunzi wamefurahi na kusherehekea kuhamishwa kwake,” alisema mmoja wa wanaharakati hao.

Hata hivyo, walisema juhudi zilizofanywa na Machibya na DC ya kufanikisha kupata mwanafunzi aliyeolewa ndoa ya kimila, lakini
akarejeshwa shuleni, zimekwama baada ya kutoroshwa tena kwenda Zanzibar.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Twatwatwa, Samwel Okeshu, amemwomba Mkuu mpya wa Mkoa, Joel Bendera, moja ya jukumu lake ni kuingilia kati kukomesha tatizo sugu la wanafunzi wa kike kuozeshwa na wazazi wao.