Get Paid To Promote, Get Paid To Popup, Get Paid Display Banner

UMEME KUPANDA BEI

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema bei ya umeme itapanda wakati wowote kuanzia sasa kutokana na Serikali na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kubeba mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji.  Katika hatua nyingine, amesema tatizo la upungufu wa umeme nchini litaendelea hadi Desemba mwaka huu na baada ya hapo litakuwa ni la kihistoria kutokana na kuwepo kwa mikakati kabambe ya kulimaliza.

Aliyasema hayo hapa alipowahutubia wakazi wa Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo. “Ni lazima bei ipande inaweza kuwa sio sasa, lakini suala la bei ya umeme kupanda lipo palepale. Kwa sasa tutaacha bei hii iendelee wakati tunaangalia tupandishe kwa kiwango gani na lini. Lakini umeme utakaokuwa unazalishwa utakuwa mwingi na wa uhakika kuliko ilivyo sasa,” alisema Pinda.

Alisema kumekuwepo na mzigo mkubwa wa bei ya umeme unaobebwa na Serikali na Tanesco kutokana na shirika hilo kutumia dola ya Marekani senti 30 kuzalisha umeme huku likiuza umeme huo kwa wananchi kwa dola ya Marekani senti 10, na hivyo kufanya Serikali kufidia nakisi inayojitokeza.  “Hatuwezi kuendelea kuiachia Tanesco mzigo huu mkubwa wa uzalishaji umeme. Lakini pia Serikali haiwezi kuendelea kuwapa Tanesco fedha kama za ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo na nyinginezo kutokana na hasara wanayopata. Ni lazima sasa bei ipande ili kukabiliana na hali hiyo,” alisema.

Akizungumzia tatizo la umeme, Pinda alisema ipo mikakati ya kuachana na umeme wa kuzalishwa kwa maji ambao ndio umekuwa unategemewa tangu Tanzania Bara ilipopata Uhuru wake mwaka 1961, uzalishaji ambao umekuwa unasababisha uhaba wa umeme wa mara kwa mara. Alisema mkakati wa sasa ni wa kutumia vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme kama kutumia makaa ya mawe, gesi asilia na upepo, vyanzo ambavyo alisema ni vya uhakika zaidi kuliko maji.

Alisema miradi kwa ajili ya upatikanaji wa umeme wa uhakika itakamilika Desemba mwaka huu na kumaliza kabisa tatizo hilo. Wakati huo huo, mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda amefanyiwa upasuaji wa pua nchini India na hali yake inaendelea vizuri. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyasema hayo mkoani hapa alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Kijiji cha Murangi katika Jimbo la Musoma Vijijini akiwa katika ziara ya kuutembelea Mkoa wa Mara.

Akishukuru kutokana na zawadi alizopewa yeye na mkewe (Tunu), Waziri Mkuu alisema imekuwa bahati mbaya kwa kushindwa kuongozana na mama Tunu kutokana na kuwa safarini India kwa matibabu. “Ziara zangu zote huambatana na mama huyu, lakini imekuwa bahati mbaya sana safari hii, maana nilipokuwa naondoka kuja huku na yeye alikuwa anaondoka kwenda India kwa matibabu.

Wataalamu walishauri aende India ili akatazamwe vizuri, alikuwa na mafua mafua hivi baadaye ikagundulika ana tatizo. “Hata hivyo nimeambiwa kuwa juzi alifanyiwa operesheni (upasuaji) na sasa hali yake inaendelea vizuri. Wakati mwingine nitakapopata bahati ya kuja Mara nitahakikisha nakuja naye,” alisema Pinda.