Bw Prosper Mugiraneza |
Waliokuwa mawaziri wawili Rwanda wamehukumiwa miaka thelathini jela na mahakama ya uhalifu wa kivita ya umoja wa mataifa kwa kujihusisha na mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.
Aliyekuwa waziri wa huduma za umma , Prosper Mugiraneza na aliyekuwa waziri wa biashara, Justin Mugenzi, walitiwa hatiani kwa kula njama ya kufanya mauaji na kuchochea mauaji hayo.
Lakini mahakama hiyo imemwachia huru aliyekuwa waziri wa afya, Casimir Bizimungu na Jerome-Clement Bicamumpaka, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wakati mauaji hayo yalipotokea, kutokana na kukosekana kwa ushahidi.
Hukumu hizo zimetolewa takriban miaka nane baada ya kesi hiyo kuanza. Pia zimetolewa miaka 12 baada ya mawaziri hao wa zamani kukamatwa. Mahakama hiyo, yenye makao yake makuu mjini Arusha nchini Tanzania, iliundwa mwaka 1994 kwa nia ya kusikiliza kesi za wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya kimbari, ambapo takriban watu 800,000, wengi wakiwa ni Watutsi waliuawa.
Katika kesi hii, wote wanne walituhumiwa kwa kuchochea mauaji ya Watutsi wakati wa mikutano ya hadhara kote nchini Rwanda na katika hotuba, baadhi ambazo zilirushwa redioni. Bw Bizimungu alikamatwa nchini Kenya Februari 1999, wakati wengine watatu walikamatwa Cameroon mwezi Aprili 1999, mahakama ilisema.