Get Paid To Promote, Get Paid To Popup, Get Paid Display Banner

Mbunge kortini, atupwa rumande

MBUNGE wa Mbarali, Modest Kilufi (CCM) amewekwa rumande katika Gereza la Ruanda jijini hapa baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama ya Mkoa wa Mbeya.

Alinyimwa dhamana hiyo na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite, Kilufi (51), baada ya kufikishwa hapo akikabiliwa na mashitaka ya kutishia kumuua Mtendaji wa Kata ya Ruiwa wilayani Mbarali, Jordan Masweve (28).

Mbunge huyo alisomewa mashitaka na mawakili wa Serikali, Griffin Mwakapeje na Basilius Namkambe mbele ya Hakimu Mteite na kudaiwa kutishia kuua Machi 16, mwaka huu katika maeneo ya Ubaruku wilayani Mbarali.

Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana mashitaka hayo na kupelekwa rumande katika Gereza la Ruanda jijini hapa baada ya dhamana yake kukataliwa na mahakama.

Hakimu alisema mbunge huyo amenyimwa dhamana kwa sababu, mahakama inatafakari kwa kina kabla ya kutoa uamuzi kutokana na unyeti wa kosa hilo.

Mbunge huyo atarudi kizimbani Oktoba 24, mwaka huu. Mshitakiwa alikamatwa na Polisi Ijumaa iliyopita saa 9 alasiri katika maeneo ya Ubaruku, kutokana na tuhuma hizo zilizokuwa zikimkabili na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana na kufikishwa mahakamani jana.

Wakati Mbunge huyo akiwekwa rumande mkoani Tabora, Mahakama imeonya kuwa itawafutia dhamana wabunge wawili wa Chadema, Sylivester Kasulumbai wa Maswa Magharibi na Suzan Kiwanga wa Viti Maalumu.

Mahakama ilitoa onyo hilo jana baada ya wabunge hao wawili kushindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili ya kumdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

Akitoa onyo hilo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Thomas Simba alisema mahakama inalazimika kutoa onyo kwa washitakiwa hao, kutokana na kutoridhika na sababu zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi.

Alisema kitendo hicho kinaonesha kuwa washitakiwa hao wanajali kazi zao na kutotoa kipaumbele kwa mahakama na kuonya wasipofika, watafutiwa dhamana ili wakae rumande.

Hakimu Simba alihoji iwapo wasingepata dhamana, wabunge hao wangepata wapi muda na ruhusa ya kuhudhuria vikao vya Kamati za Bunge.

Alisema hata kama washitakiwa hao ni wabunge wanatakiwa kuheshimu sheria na mahakama na chochote kinachotokea, wanapaswa kutoa maelezo ya sababu za kutokuhudhuria mahakamani na kuomba ruhusa, vinginevyo kesi hiyo haitaisha mapema.

Awali kabla ya onyo hilo, Wakili Mussa Kwikima, aliyewawakilisha wabunge hao pamoja na washitakiwa wenzao, aliiambia mahakama kuwa wabunge hao wameshindwa kuhudhuria mahakamani kwa sababu wako kwenye vikao vya Kamati za Bunge.

Wakili Kwikima alidai kwamba mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Anwar Kashaga, ameshindwa kuhudhuria mahakamani kwa vile yuko Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza akipatiwa matibabu.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Wakili Kwikima aliomba radhi kwa wateja wake kwa kutofika mahakamani na kuihakikishia kwamba udhuru huo hautatokea tena katika kipindi kijacho cha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa upande wa mashitaka, Juma Masanja na Mugisha Mboneko ambao walidai kuwa hoja hizo hazitoshi kuifanya mahakama ikubaliane nao kwa sababu hazina vielelezo vyovyote kama inavyotakiwa kisheria.

Mshitakiwa wa nne aliyeongezwa katika mashitaka hayo Oktoba 4, mwaka huu, Robert William, amerudishwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ya fedha taslimu Sh milioni 5 au mali isiyohamishika ya thamani hiyo na wadhamini wawili.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanashitakiwa kwa kufanya shambulio la kudhuru mwili, kuiba simu ya mkononi yenye thmani ya Sh 400,000 na kumuweka chini ya ulinzi DC huyo wa Igunga kinyume cha sheria.

Mshitakiwa Kasulumbai, mbali na mashitaka hayo, anashitakiwa kwa lugha ya kashfa dhidi ya DC Kimario.

Awali, washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, mwaka huu na kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Simba.


source: http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21889